IMANI NI KUSIKIA NA KUTII


Maandiko matakatifu yanatufundisha kuwa imani ni njia pekee ya kufikia Ufalme wa Mungu. Pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu (Waebrania 11:6). Sio kwa matoleo ya sadaka au kuhudumu katika nyumba zetu za ibada ndio tunaweza kumpendeza Mungu, bali ni kwa imani. Tafsiri ya imani ni kusikia na kutii neno litokalo kwa Kristo. Hivyo ni jukumu la kila mwanadamu kuamwamini Yesu Kristo ili kuufikia Ufalme wa Mungu.
Imani katika Yesu kristo inahusisha mambo makubwa mawili yaani usikivu na utiifu. Usikivu ni hatua ya kwanza na utiifu ni hatua ya pili katika imani ajabu ni kwamba haya Yote mawili hufanywa na Yesu kristo mwenyewe na sio kwa nguvu za binadamu.
1.   Usikivu- ni kusikia neno litokalo kwa Kristo; binadamu wote walio wateule wanauwezo wa kusikia sauti ya Mungu na pia wanauwezo wa kusikia sauti ya Yesu kristo (1Yohana 4:6). Basi imani chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo (Warumi 10:17). Maandiko matakatifu yanaonyesha awali wana wa israeli (Yakobo) taifa lililoteuliwa na Mungu walisiishi kwa kusikia sauti ya Mungu, lakini wengi waliangamizwa na wengine kupelekwa utumwani kwa sababu ya kutotii neno lake yaani sheria Yake (Warumi 10:18, Mathayo 4:4). Ndiyo sababu Yesu kristo alitumwa ulimwenguni ili kila ayasikiaye na kuyatii maneno yake asipotee bali awe na uzima wa milele (yohana 14:24)
2.   Kutii – ni kutekeleza yale maagizo yaliyo sikiwa kwa matendo. Kama ilivyo kuwa hatua ya mwanzo wa imani ni kusikia na hatua ya pili ni kutii. Basi anayeweza kulitii neno la Mungu ameitimiza imani yake na imani yake huwa kamilifu (Yakobo 2:21-22). Binadamu wanauwezo wa kusikia lakini wachache sana au hakuna wanaoweza kulitii neno la Mungu. Kwa sababu awali baba yetu Adamu alishindwa kulitii neno la Mungu. Ndomana Mungu mwenyewe aliamua kwa kupitia Yesu kristo imani yetu ianzishwe na itimizwe (waebrania 12:2).
Sasa imani huanzishwa na Yesu na inatimizwa na Yeye mwenyewe, na binadamu wanatakiwa kufahamu kuwa utimilifu wa imani katika Yesu kristo hauji kwa uwezo wa mwili bali kwa Roho mtakatifu. Wengi wanafahamu Yohana alibatiza kwa maji lakini Yesu Kristo anabatiza kwa Roho mtakatifu na kwa moto(Luka 3:16).
Adam hakuweza kutii neno la Mungu kwa maana yeye aliongozwa na tamaa za mwili; Kuja kwa Yesu kristo kulifanya imani yetu ianze maana yeye alikuja duniani akauvaa mwili kama wana wa adamu wengine lakini pia kwa kuongozwa na Roho mtakatifu aliishinda dhambi, kuzimu na mauti. Na ndiye aliepaingia patakatifu pa Mungu na katika hekalu takatifu akafanywa kuhani mkuu wa milele ambaye kwa mwili wake alifanya sadaka takatifu ya kufuta dhambi(Waebrania 10). Hii inadhihirisha kuwa Yesu kristo alikuja kurejesha uhusiano baina ya Mungu na wanadamu ambapo binadamu aliokolewa kwa mkono wa Mungu ikiwa neema na huruma zake zinatumika kutengeneza imani kama njia ya kumfikia na si kwa kuhesabiwa haki kwa matendo ya sheria (warumi 3:21-31).
Imani inampendeza Mungu na hii imekuwa njema kuliko sadaka au matoleo yaliyokuwa yanatolewa awali katika tamaduni za Israel (1 Samweli 15:22). Na pia imani yetu ni katika Yesu kristo wote wamwaminio hulisikia na kutii neno lake, kwa kufanya hivyo hukombolewa na kuimarishwa katika imani (Luka 6:46-49)  
Yesu kristo ndiye awezaye kujalia wanadamu kutii neno la Mungu; tukimwamini nakuomba kwa toba na unyenyekevu kwa Baba kwa njia yake tutapewa Roho mtakatifu (Matendo 2:38) maana Yesu ni kuhani mkuu habatizi kwa maji tu bali kwa Roho anayetuwezesha kutii neno la Mungu.
Imani humwezesha mtu kupokea baraka na nguvu za Mungu na kuuona utukufu wake (Marko 5:25-34,Yohana 11:40). Hivyo hatua ya kwanza ya imani ni kusikia neno lakini hatua ya pili ni kutii nayo huja kwa ubatizo wa Roho wa Mungu hapo imani hukamilika na huwa takatifu (Yuda1:20)


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

UHURU WA MKRISTO

MAHUSIANO NA UPENDO BAINA YA MTU NA MUNGU

SADAKA YA MOYO